Saturday, February 9, 2008

TAEKWON-DO

Taekwon-do ni sanaa ya mapambano ya kujilinda ya mikono mitupu ya asili ya Korea. Tofauti na watu wengi wanavyodhani, Taekwon-do kamwe siyo karate ya korea. Kwahiyo si sahihi kuiita sanaa hii kuwa ni karate ya korea. Karate ya Korea inaitwa Kong Soo Do ambayo ni tofauti kabisa na Taekwon-do.

Kwa bahati mbaya ufahamu wa watu wengi kuhusiana na sanaa za mapambano, (martial arts kwa lugha ya kiingereza) una misingi katika filamu. Kwenye miaka ya sabini filamu nyingi zenye kuonyesha mapambano ya aina hii zilijipatia umaarufu mkubwa sana. Jambo la kusikitisha ni kwamba watu wengi walichukulia kwamba mapigano yanayoonyeshwa kwenye filamu hizo ndio hayo yatumikayo katika hali ya kawaida, jambo ambalo si kweli kabisa. Vivyo hivyo Taekwon-do pia kama sanaa nyingine kutambulika kwake kulitokana na filamu na mashindano ya olimpiki. Hiyo ikapelekea watu wafikiri kuwa Taekwon-do ni sanaa ya mapambano ya michezo tu. Hii ni pamoja na baadhi ya walimu wa sanaa nyingine ambao wababaishaji, waliojipachika vyeo na kujiita wataalamu, wakati lengo lao ni kujipatia utajiri wa haraka kwa kudanganya watanzania wenzao na vile vile kukesha kila siku kugombea madaraka katika vyama vyao husika vya michezo badala ya kujali maendeleo ya elimu, kiwango na ufahamu wa wanamichezo wao kuhusu sanaa wanazozisimamia.

Kwanza kabisa ni lazima uelewe kuwa Taekwon-do ni tofauti na Karate, Judo, Muy Thai nakadhalika. Zote ni sanaa za mapambano lakini kuna tofauti kubwa.Mtu akichezea mpira haina maana kuwa anacheza soka, mpira wa kikapu au mpira wa mikono. Hiyo iliyotajwa hapo ni aina ya michezo ya mpira lakini yote ni tofauti katika namna ya kucheza kama vile zilivyo sanaa za mapambano.

Pili, walimu wengi wababaishaji huwadanganya watu kuwa Taekwon-do ni sanaa pekee ya mapambano ya mikono mitupu itokayo Korea. Hii si sahihi, kwani kuna sanaa nyingine nyingi zenye asili ya Korea achilia mbali Taekwon-do. Baadhi ni Kong Soo Do, Tang Soo Do, Hap Ki Do, Kuk Sool Won (inatamkwa kyuk suul wuon), Bulkyo Moo Sool, Kong Jong Moo Sool, Hoi Jeon Moo Sool, Hankido, Kumdo, Yudo na nyinginezo nyingi. Tutakuwa tunawaletea historia fupi za sanaa nyinginezo mbalimbali za Korea ili watu wapate ELIMU. Hii itajumuisha na historia ya miamba na waasisi mbalimbali wa sanaa hizo.

Tatu, wengi hudhani kuwa Taekwon-do hutegemea matumizi ya miguu tu yaani mateke katika mapambano. Ingawa kuna ukweli kidogo kuhusiana na matumizi ya miguu kwa sababu ni jambo linalofahamika kote duniani kuwa Taekwon-do ni maarufu kwa upigaji wa mateke mbali mbali lakini si kweli kuwa mateke ndio silaha pekee ya Taekwon-do. La hasha. Kuna silaha nyingi ndani ya Taekwon-do ikiwa ni pamoja na ngumi, vidole, mapigo ya mkono wazi, mapigo ya kuvunja mifupa, mapigo maalum ya kushambulia mishipa ya fahamu, umahiri wa kusokota na kuvunja mifupa na kutegua viungo, nakadhalika. Siri iliyopo hapa ni kwamba; mpiganaji wa Taekwon-do anapopewa nafasi ya kuchagua ni silaha ipi atakayokuwa tayari kuitumia kwa haraka katika pambano, basi yeye mara nyingi atachagua miguu, yaani teke. Ndio hii inapelekea watu kufikiri kuwa wapinaji wa sanaa hii wao hutumia mateke tu kwenye mapambano.

Duniani kuna vyama vikuu viwili vinavyosimamia Taekwon-do. Kuna International Taekwon-do Federation (I.T.F) na World Taekwondo Federation (W.T.F). W.T.F ndio inayo simamia Taekwon-do inayoshiriki kwenye olimpiki na I.T.F inasimamia Taekwon-do iliyoegemea kwenye mchepuo wa kujilinda ambayo hapo awali mwanzilishi na mwasisi wa Taekwon-do hiyo alikuwa ameitengeneza iwe maalum kwa ajili ya mahitaji ya wanajeshi vitani. Huyu naye alikuwa ni mwanajeshi mwenye cheo cha jenerali na aliitwa Choi Hong Hi. Sasa hivi ni marahemu. Aina hii ya Taekwon-do ni ya hatari sana kwahiyo huwa si vizuri kwa raia wasio wema kufundishwa na ndio maana inasisitiza nidhamu ya hali ya juu kama ile inayopatikana ndani ya jeshi. Kwa bahati nzuri hapa Tanzania aina hizi mbili zinapatikana.

Kuna habari zinazodai kuwa baadhi ya wadau wa sanaa hizi za mapambano ya mikono mitupu wanajenga hali ya ukaribu na ndugu zetu wa W.T.F. Si unajua kuwa mwaka huu kuna mashindano ya Olimpiki...So jamaa wanailia “taimingi” trip ya kwenda Beijing, China. Sasa sijui huko wanataka waende kama wachezaji au wasindikizaji. Sabum Prosper Makonya wa Arusha unazo hizi taarifa? Ni kweli?

No comments: