Tuesday, February 12, 2008

Kong-Soo Do

Watu wengi hufikiri kuwa Taekwon-do ni Karate ya Korea. Hii si sahihi.

Karate ya Korea inaitwa Kong Soo.

Kong-Soo Do

Historia ya sanaa hii na nyingine nyingi za Korea tunaweza kuigawa sehemu mbili;

(i) Kabla ya Uvamizi wa Wajapani { - 1910}

(ii) Baada ya Uvamizi au Wakati wa Utawala wa kikoloni wa Kijapani.

Hapa tutazungumzia (ii) zama za 1910 hadi leo.

Mnamo mwaka 1910, Majeshi ya Kijapani yalilivamia taifa la Korea na kulifanya kuwa koloni lake.
Ili kuhakikisha ya kuwa wanautokomeza utamaduni wa Kikorea wakoloni wa kijapani walifanya mambo matatu;

(i) Waliharibu na kuchoma kumbukumbu zote za kihistoria za wakorea ikiwa ni pamoja na maandiko ya mapokeo yao ya kihistoria ambayo yalijumuisha historia ya sanaa za mapigano.

(ii) Walizuia na kupiga marufuku wakorea kujifunza sanaa zao za asili ikiwa ni pamoja na zile za mapigano.

(iii) Walibadilisha mfumo wa elimu na kulazimisha mfumo wa elimu wa kijapani ndio utumike korea. Hii ni elimu kuanzia msingi, sekondari na kuendelea.

Lengo lao kuu ni kuweza kutawala kwa urahisi kwani walikuwa na imani kuwa binadamu asiye na kumbukumbu za kihistoria au asiye na utamaduni wake wa asili ni rahisi kutawaliwa.

Kilichotokea ni kwamba idadi kubwa ya vijana wa kikorea walipelekwa japani kwenda kupata elimu ya sekondati na vyuo vya juu. Huko (japani) mbali na elimu ya kawaida pia walijifunza sanaa zakijapani za mapambano ya mikono mitupu ikiwa ni pamoja na karate, jiu-jitsu, judo, kendo nakadhalika.

Mnamo mwaka 1945 wakati wa kilele cha vita kuu ya pili ya dunia, Japan ilisalimu amri kwa Marekani na washirika wake. Tukio hili pia lilimaanisha kuwa utawala wa kikoloni wa Japan huko Korea ulifika ukingoni na hivyo basi Korea ikawa ni nchi huru.

Uhuru huu ni pamoja na kuwa huru kufanya yale yote ambayo hapo awali wakoloni wakijapani waliyakataza.

Tatizo; wapi pakuanzia wakati hamna kumbukumbu?

Jambo la heri lililokuwa limetokea ni kwamba wakoloni hawakuwazuia shughuli ndogo za kitamaduni na kidini kwahiyo baadhi ya wakorea waliweza kuendelea kujifunza sanaa za mapambano ya mikono mitupu chini ya kivuli cha ngoma za asili au ibada katika mahekalu. Sanaa zilizofichwa kwa namna hii ni Tae Kyon na Soo Bakh Ki au Soo Bakh Do.

Kwahiyo utaona kwamba kuna vijana wa Korea walienda Japan kwa ajili ya masomo wakiwa tayari na ujuzi fulani wa sanaa hizi za mapigano. Pamoja na masomo yao na shughuli nyingine pia walijifunza sanaa za kijapani za mapigano.

Baada ya uhuru wakorea hao wakarudi nyumbani (Korea). Huko wakafungua shule (ninaposema shule namaanisha shule za sanaa za mapigano) na katika kujitangaza na kwa kuwa kulikuwa bado hamna sanaa za mapigano za Korea zilizokuwa hadharani wengi wakaziita sanaa zao Kong – Soo Do.

Kong-Soo Do ni tafsiri ya neno Karate-Do katika lugha ya Korea. Yaani; yale maandishi ya kijapani ambayo husomeka Karate-Do kwa kikorea tafsiri ya neno hilo linatamkwa “Kong-Soo Do”.

Mitindo (Style) mingi ya Kong-Soo (Karate) ilianza kufundishwa, mojawapo ya mitindo hiyo ni “Song Moo Kwan”.

Song Moo Kwan ni matamko ya kikorea ya neno Shotokan.

Tanzania kuna mitindo mbalimbali ya Karate, ila yenye wafuasi wengi ni Shotokan na Goju-ryu.

Muasisi wa “Song Moo Kwan” anaitwa Byung Rick Ro. Huyu alizaliwa tarehe 3 Julai, 1919 huko Kaesung, Korea. Akiwa mtoto, umri wa miaka yapata 12 hivi alianza kuhudhuria mafunzo ya sanaa zilizokuwa zinafundishwa kwa kificho chini ya mwamvuli wa ibada kwenye hekalu lililokuwa jirani na nyumbani kwao. Sanaa alizojifunza zilikuwa Soo Bakh Kin na Tae Kyon. Alipotimiza miaka 17 alikwenda Japan kwa ajili ya masomo. Huku akiendelea na masomo kwenye chuo kilichokuwa kinaitwa Chou, alianza pia kujifunza Shotokan Karate chini ya muasisi wa sanaa hiyo, Gichin Funakoshi.

Mnamo tarehe 2 Mei, 1946, Byung Rick Ro alifungua rasmi shule na kuuita mtindo aliokuwa anafundisha “Song Moo Kwan Kong-Soo Do”. Alichukua yale aliyofundishwa na Funakoshi akaongeza mapokeo kutoka kwenye Tae Kyon na Soo Bakh Ki akatengeneza Song Moo. Kwahiyo si kwamba Song Moo Kwan ni Shotokan toka nitoke..hapana. Zinafanana baadhi ya misingi na kwamba zote zinatumia jina moja katika lugha mbili tofauti, sawa na kusema Musa na Moses au John na Yohana. Tofauti nyingine ni kwamba kutokana na mapokeo ya Taekyon kuwepo ndani ya Song Moo Kwan utaona kwamba ina miondoko inyofuata umbo la duara wakati Shotokan ni mtindo mnyofu. Hauna maduara.

Bahati mbaya maendeleo ya mfumo wake chini ya jina hili hayakuwa mazuri. Hii ilisababishwa na mambo makuu mawili:-

(i) Korea ndio imepata uhuru kwahiyo wakorea hawakupenda kujihusisha na ambacho kingewakumbusha utawala wa kikoloni wa wajapani. Pia kwa kuwa Song Moo Kwan ilikuwa ni tafsiri ya herufi za kijapani zinazotumika kuandika neno Shotokan utaifa uliingia na hivyo kufanya Song Moo Kwan kuonekana kana kwamba ni mapokeo ya utamaduni wa kijapani.

(ii) Korea kama taifa iliingia kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vilisababisha Korea kugawanyika kuwa Korea kusini na Korea kaskazini. Hali hii ilisababisha shule nyingi za sanaa za mapigano kufungwa huku walimu na wanafunzi wakiitwa jeshini.

Kutokana na hayo Kong-Soo Do ikafifia.

Mitindo mbalimbali iliyokuwa inaitwa Kong Soo ikatoweka au kubadilisha majina na kumezwa na mtindo mpya uliokuja kujulikana kama Tang-Soo Do.

Baadhi shule za mwanzo za Kong Soo Do ukiachia mbali Song Moo Kwan ni Chung Do Kwan, Chang Moo Kwan, Yun Moo Kwan, Ji Do Kwan nakadhalika.

Leo hii kuna shule chache mno zinazofundisha sanaa inayoitwa Kong-Soo Do.

No comments: